13 Jihadharini msitoe sadaka zenu za kuteketezwa mahali popote mnapopaona;
14 bali katika mahali atakapopachagua Mwenyezi-Mungu katika mojawapo ya makabila yenu. Hapo ndipo mtakapotoa sadaka zenu za kuteketezwa, na ndipo mtakapofanyia mambo yote niliyowaamuru.
15 “Lakini mna uhuru wa kuchinja na kula wanyama wenu popote katika makao yenu mnavyopenda, kama baraka za Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, alizowapa, kadiri mtakavyojaliwa na Mwenyezi-Mungu. Watu wote, walio safi au najisi wanaweza kula nyama hizo, kama vile mlavyo nyama ya paa au ya kulungu.
16 Lakini msile damu ya wanyama hao; imwageni damu hiyo ardhini kama maji.
17 Msile vitu vifuatavyo mahali mnapoishi: Zaka ya nafaka zenu, wala ya divai yenu, wala ya mafuta yenu, wala ya wazaliwa wa kwanza wa ng'ombe au kondoo wenu, wala sadaka zenu za nadhiri au tambiko zenu za hiari, wala matoleo mengineyo.
18 Mtavila vitu hivyo mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mahali atakapopachagua Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu. Mtavila nyinyi pamoja na watoto wenu wa kiume na wa kike, watumishi wenu wa kiume na wa kike, na Walawi wanaoishi katika miji yenu.
19 Pia hakikisheni kwamba hamtawasahau Walawi muda wote mtakaoishi katika nchi yenu.