26 Vitu vitakatifu mtakavyotoa na sadaka zenu za nadhiri, mtavichukua na kuvipeleka mahali Mwenyezi-Mungu atakapochagua.
27 Hapo, mtatoa sadaka za kuteketezwa, nyama na damu, kwenye madhabahu ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu; damu ya mnyama mtainyunyiza kwenye madhabahu yake Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, lakini mnaruhusiwa kula nyama.
28 Jihadharini kutii maneno haya niliyowaamuru, ili mpate kufanikiwa nyinyi pamoja na wazawa wenu baada yenu milele, maana mtakuwa mnatenda yaliyo mema na yaliyo sawa mbele ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.
29 “Baada ya Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kuyakatilia mbali mataifa mbele yenu, hayo ambayo mnakwenda kuyafukuza, kuyatoa na kukaa katika nchi yao,
30 jihadharini msijiingize mtegoni kwa kuyafuata baada ya kuangamizwa mbele yenu. Msijisumbue kujua kuhusu miungu yao, mkisema, ‘Mataifa haya yaliabuduje miungu yake? – ili nasi tuwaabudu vivyo hivyo’.
31 Msimwabudu hivyo Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kwa maana kila chukizo ambalo Mwenyezi-Mungu hapendi, wameifanyia miungu yao; hata wamewachoma motoni watoto wao wa kiume na wa kike, ili kuitambikia miungu yao.
32 “Hakikisheni kwamba mmefanya kila kitu nilichowaamuru; msiongeze kitu wala msipunguze kitu.