1 Uwe mwangalifu uendapo katika nyumba ya Mungu, na kukaribia ili kusikiliza kwa makini kuliko kutambika kama watambikavyo wapumbavu, watu wasiopambanua kati ya jema na ovu.
2 Fikiri kabla ya kusema, wala usiwe mwepesi kusema chochote mbele ya Mungu, kwa maana Mungu yuko mbinguni na wewe uko duniani. Kwa hiyo usiseme mengi.
3 Kadiri mtu anavyohangaika zaidi, ndivyo atakavyoota ndoto;sauti ya mpumbavu ni maneno mengi.
4 Ukimwekea Mungu nadhiri, usikawie kuitimiza; na Mungu hapendezwi na wapumbavu. Tekeleza ulichoahidi.
5 Ni afadhali kutoweka nadhiri kuliko kuweka nadhiri kisha usiitimize.
6 Angalia mdomo wako usikuingize dhambini, halafu ikupase kumwambia mjumbe wa Mungu kwamba hukunuia kutenda dhambi. Ya nini kumfanya Mungu akukasirikie na kuiharibu kazi yako?
7 Ndoto zikizidi, kuna maangamizi na maneno huwa mengi. Jambo la maana ni kumcha Mungu.