Mhubiri 10 BHN

1 Nzi waliokufa husababisha marashi kunuka;upumbavu kidogo hubatilisha hekima na heshima.

2 Moyo wa mwenye hekima humwongoza kutenda yaliyo sawa;lakini mtu mpumbavu moyo wake humpotosha.

3 Hata apitapo njiani, mpumbavu hutambulikana hivyo,humjulisha kila mtu kwamba yeye ni mpumbavu.

4 Mtawala akikuwakia hasira, usijiuzulu;makosa makubwa huweza kufutwa ukiwa mnyenyekevu.

5 Kuna uovu niliogundua hapa duniani, uovu unaosababishwa na watawala:

6 Kwamba wapumbavu wanapewa kazi za madaraka ya juu, na matajiri wanachukua nafasi za mwisho.

7 Nimeona watumwa wanapanda farasi, na wakuu wanatembea kwa miguu kama watumwa.

8 Mchimba shimo hutumbukia mwenyewe,abomoaye ukuta huumwa na nyoka.

9 Mchonga mawe huumizwa nayo,mkata kuni hukabiliwa na hatari.

10 Nguvu nyingi zaidi zahitajikakwa mtumiaji shoka butu lisilonolewa,lakini kutumia hekima humfanya mtu afanikiwe.

11 Nyoka akiuma kabla hajachochewa,mchochezi hahitajiki tena.

12 Maneno ya mwenye hekima humnufaisha asemaye;lakini midomo ya mpumbavu humwangamiza.

13 Mpumbavu huanza kusema kwa maneno ya kijinga,na kumaliza kauli yake kwa wazimu mbaya.

14 Mpumbavu hububujika maneno.Binadamu hajui yatakayokuwako,wala yale yatakayotukia baada yake.

15 Mpumbavu huchoshwa na kazi yakehata asijue njia ya kurudia nyumbani.

16 Ole wako, ewe nchi, mtawala wako akiwa kijana,na viongozi wako wakifanya sherehe asubuhi.

17 Heri yako, ewe nchi, mtawala wako akiwa mtu wa heshima,na viongozi wako wakifanya sherehe wakati wa kufaa,ili kujipatia nguvu na si kujilewesha.

18 Kutokana na uvivu wa mtu, paa hubonyea;kwa sababu ya uzembe, nyumba huvuja.

19 Chakula ni kwa ajili ya kujifurahisha,divai huchangamsha maisha;na fedha husababisha hayo yote.

20 Usimwapize mtawala hata moyoni mwako,wala usimwapize tajiri hata chumbani mwako unakolala,kwa kuwa ndege ataisikia sauti yako,au kiumbe arukaye atatangaza maneno yako.

Sura

1 2 3 4 5 6 7 8 9 10 11 12