1 Umkumbuke Muumba wako siku za ujana wako,kabla hazijaja siku na miaka ambapo utasema:“Sifurahii tena vitu hivyo!”
2 Umkumbuke kabla ya wakati ambapo kwako mwanga wa jua utafifia;mwezi na nyota haviangazi tena,nayo mawingu yametanda tena baada ya mvua.
3 Wakati ambapo mikono inayokulinda inatetemeka,miguu yako imara imepindika,meno yako ya kusagia hayafai kwa uchache,na macho ya kuchungulia dirishani yamefifia.
4 Wakati ambapo milango ya masikio yako imezibika,na sauti za visagio ni hafifu;lakini usiku hata kwa sauti ya ndege utagutuka.
5 Wakati huo utaogopa kupanda mahali pa juuna kutembea barabarani ni kitisho;wakati miti ya mlozi inachanua na panzi wanashiba,lakini wewe hutakuwa na hamu tena.Wakati huo binadamu anapaswa kwenda katika makao yake ya milele,nao waombolezaji watapitapita barabarani.
6 Wakati huo uzi wa dhahabu utakatika,bakuli la dhahabu litapasuka,mtungi wa maji utavunjikia kisimani,kadhalika na gurudumu la kuvutia maji.
7 Nawe vumbi utarudia udongoni ulimotolewana roho yako itamrudia Mungu aliyeiumba.
8 Mimi Mhubiri nasema: Yote ni bure kabisa! Yote ni bure.
9 Basi, zaidi ya kuwa na hekima yake, Mhubiri aliwafundisha watu ujuzi. Alizipima, akazichunguza na kuzirekebisha methali kwa ustadi mwingi.
10 Mhubiri alijitahidi kupata maneno ya kupendeza, akaandika kwa ufasaha maneno ya kweli.
11 Misemo ya wenye hekima ni kama michokoo na methali zilizokusanywa pamoja na mchungaji mmoja ni kama vigingi vilivyopigiliwa imara ardhini.
12 Zaidi ya hayo, mwanangu, jihadhari! Kuandika vitabu hakuna mwisho na kusoma kwingi huchokesha mwili.
13 Baada ya hayo yote yaliyokwisha semwa bado kuna hili linalotakiwa: Mche Mungu, na uzishike amri zake; kwa sababu hilo ndilo jukumu aliloumbiwa binadamu.
14 Maana, Mungu atahukumu matendo yetu yote, hata yale yanayotendwa kwa siri, yawe mema au mabaya.