1 Laiti ungekuwa kaka yangu,ambaye amenyonyeshwa na mama yangu!Hivyo, hata kama ningekutana nawe nje,ningekubusu na hakuna ambaye angenidharau.
2 Ningekuongoza na kukufikisha nyumbani kwa mama mzazi,mahali ambapo ungenifundisha upendo.Ningekupa divai nzuri iliyokolezwa,ningekupa divai yangu ya makomamanga yangu.
3 Mkono wako wa kushoto u chini ya kichwa changu,na mkono wako wa kulia wanikumbatia.
4 Nawasihini, enyi wanawake wa Yerusalemu,msiyachochee wala kuyaamsha mapenzi,hadi hapo wakati wake utakapofika.
5 Ni nani huyu ajaye kutoka mbugani,huku anamwegemea mpenzi wake?Chini ya mtofaa, mimi nilikuamsha,pale ambapo mama yako aliona uchungu,naam, pale ambapo mama yako alikuzaa.
6 Nipige kama mhuri moyoni mwako,naam, kama mhuri mikononi mwako.Maana pendo lina nguvu kama kifo,wivu nao ni mkatili kama kaburi.Mlipuko wake ni kama mlipuko wa moto,huwaka kama mwali wa moto.
7 Maji mengi hayawezi kamwe kulizima,mafuriko hayawezi kulizamisha.Mtu akijaribu kununua pendo,akalitolea mali yake yote,atakachopata ni dharau tupu.