1 Mfalme Adoni-sedeki wa Yerusalemu alipata habari juu ya jinsi Yoshua alivyouteka mji wa Ai na kuuharibu kabisa akiutendea mji huo na mfalme wake kama alivyoutendea Yeriko na mfalme wake. Pia alipata habari kwamba wakazi wa Gibeoni walikuwa wamefanya mkataba wa amani na Waisraeli na kwamba sasa wanaishi miongoni mwao.
2 Habari hizo zilisababisha hofu kubwa huko Yerusalemu kwa sababu mji wa Gibeoni ulikuwa maarufu miongoni mwa miji ya kifalme. Isitoshe, mji huu ulikuwa maarufu kuliko Ai na wanaume wake wote walikuwa askari hodari mno.
3 Basi, Mfalme Adoni-sedeki akapeleka ujumbe kwa mfalme Hohamu wa Hebroni, mfalme Piramu wa Yarmuthi, mfalme Yafia wa Lakishi na mfalme Debiri wa Egloni, akawaambia,
4 “Njoni mnisaidie tuwaangamize Wagibeoni, maana wamefanya mkataba wa amani na Yoshua pamoja na Waisraeli.”
5 Kisha wafalme hao watano wa Waamori: Mfalme wa Yerusalemu, mfalme wa Hebroni, mfalme wa Yarmuthi, mfalme wa Lakishi na mfalme wa Egloni, wakaunganisha majeshi yao, wakaenda nayo mpaka Gibeoni; wakapiga kambi kuuzingira mji huo, wakaushambulia.
6 Wagibeoni wakapeleka ujumbe kwa Yoshua huko kambini Gilgali, wakamwambia, “Tafadhali, usitutupe sisi watumishi wako; njoo upesi utusaidie na kutuokoa kwa maana wafalme wote wa Waamori kutoka nchi ya milimani wamekuja kutushambulia.”