34 Kisha kutoka Lakishi, Yoshua na Waisraeli wote walikwenda mpaka Egloni, wakauzingira na kuushambulia.
35 Wakauteka siku hiyohiyo na kuwaua wakazi wake wote kama walivyofanya kule Lakishi.
36 Halafu kutoka Egloni Yoshua na Waisraeli wote wakaenda mpaka Hebroni, wakaushambulia
37 na kuuteka. Wakawaua wakazi wake wote pamoja na mfalme wao; waliiharibu kabisa miji mingine iliyouzunguka, wakawaua wakazi wake wote kama walivyofanya kule Egloni.
38 Kisha, Yoshua na Waisraeli wote wakarudi Debiri, wakaushambulia.
39 Waliuteka mji huo na mfalme wake pamoja na miji mingine yote iliyouzunguka na kuwaangamiza wote waliokuwamo bila kumbakiza hata mtu mmoja. Waliutendea mji huo kama walivyoutendea mji wa Hebroni na mji wa Libna na wafalme wao.
40 Basi, Yoshua aliiteka nchi yote; aliwashinda wafalme wa sehemu za milimani, eneo la Negebu, na sehemu za nchi tambarare na miteremko. Hakuacha chochote chenye uhai ila aliangamiza kila kitu kama Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, alivyoamuru.