6 pia eneo la milima iliyo kati ya Lebanoni na Misrefoth-maimu ambayo wakazi wake ni Wasidoni. Kadiri Waisraeli watakavyoendelea katika nchi hizo, mimi mwenyewe nitayafukuza mataifa hayo mbele yao. Nawe utawagawia Waisraeli sehemu mbalimbali za nchi hizo kwa kura kama nilivyokuamuru.
7 Utayagawia nchi hizo makabila tisa na nusu ya kabila la Manase ambayo bado hayajapata kitu.”
8 Makabila ya Reubeni, Gadi na nusu nyingine ya kabila la Manase yalikuwa yamepewa nchi iliyo mashariki ya mto Yordani, kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose, mtumishi wake.
9 Eneo lao lilikuwa kuanzia Aroeri ukingoni mwa bonde la Arnoni na mji ule ulio katikati ya bonde, na nchi ile yote ya tambarare tangu Medeba mpaka Diboni,
10 pamoja na miji ya mfalme Sihoni wa Waamori, aliyetawala huko Heshboni hadi mpakani mwa Waamoni,
11 pamoja na nchi za Gileadi, eneo la Wageshuri na Wamaakathi, mlima wa Hermoni na nchi yote ya Bashani mpaka Saleka;
12 na ufalme wote wa Ogu mmoja wa Warefai waliosalia, ambaye alitawala huko Ashtarothi na Edrei katika Bashani. Mose alikuwa amewashinda hao wote na kuwafukuzia mbali.