1 Yafuatayo ni maeneo ya nchi ambayo walipewa Waisraeli katika nchi ya Kanaani. Kuhani Eleazari na Yoshua, mwana wa Nuni, pamoja na wakuu wa koo za makabila ya Waisraeli waliwagawia Waisraeli.
2 Sehemu yao hiyo waligawiwa kwa kura kama vile Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose awape yale makabila tisa na nusu.
3 Mose alikuwa ameyapa yale makabila mawili na nusu sehemu yao mashariki ya Yordani, lakini Walawi hawakuwa wamepewa sehemu yao pamoja nao.
4 Wazawa wa Yosefu walikuwa makabila mawili: Manase na Efraimu. Kabila la Lawi halikupewa sehemu yoyote ya nchi, ila miji tu ya kuishi na sehemu za malisho kwa ajili ya wanyama wao na riziki zao.