10 Huko Shilo, Yoshua akazipigia kura sehemu hizo mbele ya Mwenyezi-Mungu, akawagawia Waisraeli; kila kabila na sehemu yake.
11 Kura ya kwanza ililipata kabila la Benyamini kulingana na koo zake. Eneo walilopewa watu hao lilikuwa katikati ya lile la kabila la Yuda na lile la kabila la Yosefu.
12 Mpaka wake wa kaskazini ulianzia mto Yordani na kupitia kaskazini mwa Yeriko na nchi ya milima ukaelekea magharibi hadi kwenye nyika ya Beth-aveni.
13 Kutoka huko, mpaka wake ulikwenda kusini kuelekea Luzu kupitia upande wa kusini wa Luzu (yaani Betheli) hadi Ataroth-adari, kwenye mlima ulioko kusini mwa Beth-horoni ya Chini.
14 Upande wa magharibi wa mlima huo ulio kusini mwa Beth-horoni mpaka uligeuka ukaelekea kusini hadi Kiriath-baali, uitwao pia Kiriath-yearimu, mji ambao ni mali ya kabila la Yuda. Huu ndio uliokuwa mpaka wake upande wa magharibi.
15 Upande wa kusini mpaka wake ulianzia kwenye viunga vya mji wa Kiriath-yearimu, ukafika Efroni na kwenda hadi kwenye chemchemi ya maji ya Neftoa.
16 Kisha ulielekea chini kupitia pembeni mwa mlima ulioko karibu na bonde la mwana wa Hinomu, ambalo lilikuwa katika sehemu ya kaskazini zaidi ya bonde la Warefai. Halafu mpaka uliteremka kuelekea bonde la Hinomu, kusini mwa kilima cha Wayebusi, ukaendelea kuteremka hadi En-rogeli.