8 Basi, watu hao wakaanza safari ya kwenda kuichunguza nchi. Kabla hawajaenda, Yoshua akawapa maagizo: “Nendeni nchini kote mkaandike maelezo kamili juu ya hiyo nchi, kisha mrudi mnieleze, nami nitapiga kura mbele ya Mwenyezi-Mungu hapa hapa Shilo kuhusu sehemu mtakayopewa.”
9 Wanaume hao wakazunguka nchini kote, wakachora maelezo kamili juu ya sehemu zake saba pamoja na miji yake, kisha wakarudi kwa Yoshua kule kambini Shilo.
10 Huko Shilo, Yoshua akazipigia kura sehemu hizo mbele ya Mwenyezi-Mungu, akawagawia Waisraeli; kila kabila na sehemu yake.
11 Kura ya kwanza ililipata kabila la Benyamini kulingana na koo zake. Eneo walilopewa watu hao lilikuwa katikati ya lile la kabila la Yuda na lile la kabila la Yosefu.
12 Mpaka wake wa kaskazini ulianzia mto Yordani na kupitia kaskazini mwa Yeriko na nchi ya milima ukaelekea magharibi hadi kwenye nyika ya Beth-aveni.
13 Kutoka huko, mpaka wake ulikwenda kusini kuelekea Luzu kupitia upande wa kusini wa Luzu (yaani Betheli) hadi Ataroth-adari, kwenye mlima ulioko kusini mwa Beth-horoni ya Chini.
14 Upande wa magharibi wa mlima huo ulio kusini mwa Beth-horoni mpaka uligeuka ukaelekea kusini hadi Kiriath-baali, uitwao pia Kiriath-yearimu, mji ambao ni mali ya kabila la Yuda. Huu ndio uliokuwa mpaka wake upande wa magharibi.