1 Basi, Yoshua, mwana wa Nuni, akawatuma watu wawili kwa siri kutoka Shitimu waende kufanya upelelezi, katika nchi ile na hasa mji wa Yeriko. Wakaenda, wakafika kwenye nyumba ya malaya mmoja aliyeitwa Rahabu wakalala humo.
2 Mfalme wa mji wa Yeriko akaambiwa, “Tazama, wanaume wawili Waisraeli wameingia mjini leo usiku ili kuipeleleza nchi.”
3 Mfalme wa Yeriko akatuma watu kwa Rahabu, akisema: “Watoe nje watu waliokuja nyumbani kwako kwani wamekuja kuipeleleza nchi yote.”
4 Lakini, yule mwanamke alikuwa amekwisha waficha watu hao wawili. Basi, akawaambia wajumbe hao, “Ni kweli kwamba hao watu walikuja kwangu, lakini mimi sikujua wametoka wapi.