21 Hapo watu wa makabila ya Reubeni na Gadi na nusu ya kabila la Manase wakawajibu viongozi wa jamaa za Israeli,
22 “Mungu wa miungu ndiye Mwenyezi-Mungu! Mungu wa miungu ndiye Mwenyezi-Mungu! Yeye anajua kwa nini tumefanya hivyo. Na Waisraeli wote watajua pia! Kama huu ni uasi au ni ukosefu wa imani kwa Mwenyezi-Mungu basi, yeye aache kutuokoa leo.
23 Kama tumemwacha Mwenyezi-Mungu tukajenga madhabahu yetu wenyewe ili tutoe sadaka za kuteketezwa, za nafaka au za amani, basi Mwenyezi-Mungu na atulipize kisasi.
24 Lakini sivyo ilivyo. Tuliijenga kwa kuogopa kwamba huenda katika siku zijazo watoto wenu watawaambia watoto wetu, ‘Nyinyi mna uhusiano gani na Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli?
25 Hamwoni kwamba Mwenyezi-Mungu ameweka mto wa Yordani kuwa mpaka kati yenu na sisi? Nyinyi makabila ya Reubeni na kabila la Gadi hamna fungu lolote lenu kwa Mwenyezi-Mungu.’ Hivyo watoto wenu wangeweza baadaye kusababisha watoto wetu waache kumwabudu Mwenyezi-Mungu.
26 Ndiyo maana tuliamua kujenga madhabahu hii, lakini si kwa ajili ya kutolea juu yake sadaka wala tambiko,
27 bali tulitaka madhabahu hii iwe ushuhuda kati yetu na nyinyi na vizazi vyetu vijavyo kwamba sisi tunayo haki ya kumtumikia Mwenyezi-Mungu kwa sadaka zetu za kuteketezwa na tambiko zetu, na kwa sadaka zetu za amani, ili watoto wenu wasije wakawaambia watoto wetu kwamba hawana fungu lolote lao kwa Mwenyezi-Mungu.