1 Kisha Yoshua akayakusanya makabila yote ya Israeli huko Shekemu. Akawaita wazee, viongozi, waamuzi na maofisa wa Israeli, nao wakaja mbele ya Mungu.
2 Yoshua akawaambia watu wote, “Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, asema hivi: Hapo zamani, wazee wenu waliishi ngambo ya mto Eufrate, wakaitumikia miungu mingine. Mzee mmoja alikuwa Tera, baba yao Abrahamu na Nahori.
3 Mimi Mungu nilimwondoa babu yenu Abrahamu kutoka huko ngambo ya mto Eufrate na kumleta hapa Kanaani, ambako nilimpatia wazawa wengi. Nilimpa Isaka,
4 naye Isaka nikampa Yakobo na Esau. Nilimpa Esau milima ya Seiri aimiliki. Lakini Yakobo na watoto wake walikwenda Misri.