4 Yeye anenaye kwa lugha hujijenga nafsi yake; bali ahutubuye hulijenga kanisa.
5 Nami nataka ninyi nyote mnene kwa lugha, lakini zaidi sana mpate kuhutubu, maana yeye ahutubuye ni mkuu kuliko yeye anenaye kwa lugha, isipokuwa afasiri, ili kusudi kanisa lipate kujengwa.
6 Ila sasa, ndugu, nikija kwenu na kunena kwa lugha, nitawafaidia nini, isipokuwa nasema nanyi kwa njia ya ufunuo, au kwa njia ya elimu, au kwa njia ya hotuba, au kwa njia ya fundisho?
7 Hata vitu visivyo na uhai vitoapo sauti, ikiwa ni filimbi, ikiwa ni kinubi, visipotoa sauti zilizo na tofauti, itatambulikanaje ni wimbo gani unaopigwa kwa filimbi au kwa kinubi?
8 Kwa maana baragumu ikitoa sauti isiyojulikana, ni nani atakayejifanya tayari kwa vita?
9 Vivyo hivyo na ninyi, msipotoa kwa ulimi neno lililo dhahiri, neno lile linenwalo litajulikanaje? Maana mtakuwa mkinena hewani tu.
10 Yamkini ziko sauti za namna nyingi duniani, wala hakuna moja isiyo na maana.