1 Basi, ndugu zangu, mimi nilipokuja kwenu, sikuja niwahubiri siri ya Mungu kwa ufasaha wa maneno, wala kwa hekima.
2 Maana naliazimu nisijue neno lo lote kwenu ila Yesu Kristo, naye amesulibiwa.
3 Nami nalikuwako kwenu katika hali ya udhaifu na hofu na matetemeko mengi.
4 Na neno langu na kuhubiri kwangu hakukuwa kwa maneno ya hekima yenye kushawishi akili za watu, bali kwa dalili za Roho na za nguvu,
5 ili imani yenu isiwe katika hekima ya wanadamu, bali katika nguvu za Mungu.
6 Walakini iko hekima tusemayo kati ya wakamilifu; ila si hekima ya dunia hii, wala ya hao wanaoitawala dunia hii, wanaobatilika;
7 bali twanena hekima ya Mungu katika siri, ile hekima iliyofichwa, ambayo Mungu aliiazimu tangu milele, kwa utukufu wetu;
8 ambayo wenye kuitawala dunia hii hawaijui hata mmoja; maana kama wangaliijua, wasingalimsulibisha Bwana wa utukufu;
9 lakini, kama ilivyoandikwa,Mambo ambayo jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia,(Wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu,)Mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao.
10 Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu.
11 Maana ni nani katika binadamu ayajuaye mambo ya binadamu ila roho ya binadamu iliyo ndani yake? Vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu.
12 Lakini sisi hatukuipokea roho ya dunia, bali Roho atokaye kwa Mungu, makusudi tupate kuyajua tuliyokirimiwa na Mungu.
13 Nayo twayanena, si kwa maneno yanayofundishwa kwa hekima ya kibinadamu, bali yanayofundishwa na Roho, tukiyafasiri mambo ya rohoni kwa maneno ya rohoni.
14 Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni.
15 Lakini mtu wa rohoni huyatambua yote, wala yeye hatambuliwi na mtu.
16 Maana, Ni nani aliyeifahamu nia ya Bwana, amwelimishe? Lakini sisi tunayo nia ya Kristo.