6 Labda nitakaa kwenu; naam, labda wakati wote wa baridi, mpate kunisafirisha ko kote nitakakokwenda.
7 Maana sipendi kuonana nanyi sasa, katika kupita tu, kwa sababu nataraji kukaa kwenu muda kidogo, Bwana akinijalia.
8 Lakini nitakaa Efeso hata Pentekoste;
9 kwa maana nimefunguliwa mlango mkubwa wa kufaa sana, na wako wengi wanipingao.
10 Lakini, Timotheo akija, angalieni akae kwenu pasipo hofu; maana anaifanya kazi ya Bwana vile vile kama mimi mwenyewe;
11 basi mtu ye yote asimdharau, lakini msafirisheni kwa amani, ili aje kwangu; maana ninamtazamia pamoja na ndugu zetu.
12 Lakini kwa habari za Apolo, ndugu yetu, nalimsihi sana aende kwenu pamoja na hao ndugu; ambaye si mapenzi yake kwenda sasa; lakini atakuja atakapopata nafasi.