5 Kwa maana hatujihubiri wenyewe, bali Kristo Yesu ya kuwa ni Bwana; na sisi wenyewe kuwa tu watumishi wenu kwa ajili ya Yesu.
6 Kwa kuwa Mungu, aliyesema, Nuru itang’aa toka gizani, ndiye aliyeng’aa mioyoni mwetu, atupe nuru ya elimu ya utukufu wa Mungu katika uso wa Yesu Kristo.
7 Lakini tuna hazina hii katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu, wala si kutoka kwetu.
8 Pande zote twadhikika, bali hatusongwi; twaona shaka, bali hatukati tamaa;
9 twaudhiwa, bali hatuachwi; twatupwa chini, bali hatuangamizwi;
10 siku zote twachukua katika mwili kuuawa kwake Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu.
11 Kwa maana sisi tulio hai, siku zote twatolewa tufe kwa ajili ya Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu ipatikanayo na mauti.