2 tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Mungu.
3 Maana mtafakarini sana yeye aliyeyastahimili mapingamizi makuu namna hii ya watendao dhambi juu ya nafsi zao, msije mkachoka, mkizimia mioyoni mwenu.
4 Hamjafanya vita hata kumwagika damu, mkishindana na dhambi;
5 tena mmeyasahau yale maonyo, yasemayo nanyi kama kusema na wana,Mwanangu, usiyadharau marudia ya Bwana,Wala usizimie moyo ukikemewa naye;
6 Maana yeye ambaye Bwana ampenda, humrudi,Naye humpiga kila mwana amkubaliye.
7 Ni kwa ajili ya kurudiwa mwastahimili; Mungu awatendea kama wana; maana ni mwana yupi asiyerudiwa na babaye?
8 Basi kama mkiwa hamna kurudiwa, ambako ni fungu la wote, ndipo mmekuwa wana wa haramu ninyi, wala si wana wa halali.