15 Ndugu zangu, nanena kwa jinsi ya kibinadamu. Lijapokuwa ni agano la mwanadamu, hata hivyo likiisha kuthibitika, hakuna mtu alibatilishaye, wala kuliongeza neno.
16 Basi ahadi zilinenwa kwa Ibrahimu na kwa mzao wake. Hasemi, Kwa wazao, kana kwamba ni wengi, bali kana kwamba ni mmoja, Kwa mzao wako, yaani, Kristo.
17 Nisemalo ni hili; agano lililothibitishwa kwanza na Mungu, torati iliyotokea miaka mia nne na thelathini baadaye hailitangui, hata kuibatilisha ile ahadi.
18 Kwa maana urithi ukiwa kwa sheria, hauwi tena kwa ahadi; lakini Mungu alimkirimia Ibrahimu kwa njia ya ahadi.
19 Torati ni nini basi? Iliingizwa kwa sababu ya makosa, hata aje huyo mzao aliyepewa ile ahadi; iliamriwa kwa utumishi wa malaika kwa mkono wa mjumbe.
20 Basi aliye mjumbe si mjumbe wa mmoja; bali Mungu ni mmoja.
21 Basi je! Torati haipatani na ahadi za Mungu? Hasha! Kwa kuwa, kama ingalitolewa sheria iwezayo kuhuisha, yakini haki ingalipatikana kwa sheria.