1 Akaanza kusema nao kwa mifano; Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu, akazungusha ugo, akachimba shimo la shinikizo, akajenga mnara, akapangisha wakulima, akasafiri.
2 Hata kwa wakati wake akatuma mtumwa kwa wale wakulima, ili apokee kwa wakulima katika matunda ya mizabibu.
3 Wakamtwaa, wakampiga, wakamtoa nje, hana kitu.
4 Akatuma tena kwao mtumwa mwingine, na huyo wakamtia jeraha za kichwa, wakamfanyia jeuri.
5 Akamtuma mwingine, huyo wakamwua; na wengine wengi, hawa wakiwapiga na hawa wakiwaua.
6 Basi alikuwa na mmoja bado, mwana mpendwa wake; huyu naye akamtuma kwao mwisho, akisema, Watamstahi mwanangu.
7 Lakini wale wakulima wakasemezana, Huyu ni mrithi; haya, na tumwue, na urithi utakuwa wetu.