6 Akawaambia, Litupeni jarife upande wa kuume wa chombo, nanyi mtapata. Basi wakatupa; wala sasa hawakuweza kulivuta tena kwa sababu ya wingi wa samaki.
7 Basi yule mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda akamwambia Petro, Ndiye Bwana. Naye Simoni Petro, aliposikia ya kwamba ni Bwana, akajifunga vazi lake, (maana alikuwa uchi), akajitupa baharini.
8 Na hao wanafunzi wengine wakaja katika mashua; maana hawakuwa mbali na nchi kavu; ila yapata dhiraa mia mbili; huku wakilikokota lile jarife lenye samaki.
9 Basi waliposhuka pwani, wakaona huko moto wa makaa, na juu yake pametiwa samaki, na mkate.
10 Yesu akawaambia, Leteni hapa baadhi ya samaki mliowavua sasa hivi.
11 Basi Simoni Petro akapanda chomboni, akalivuta jarife pwani, limejaa samaki wakubwa, mia hamsini na watatu; na ijapokuwa ni wengi namna hiyo, jarife halikupasuka.
12 Yesu akawaambia, Njoni mfungue kinywa. Wala hakuna mtu katika wale wanafunzi aliyethubutu kumwuliza, U nani wewe? Wakijua ya kuwa ni Bwana.