12 Walakini katika siku zako sitafanya haya, kwa ajili ya Daudi baba yako; nitaurarua utoke katika mkono wa mwana wako.
13 Lakini sitauondoa ufalme wote pia; nitampa mwana wako kabila moja, kwa ajili ya Daudi mtumishi wangu, na kwa ajili ya Yerusalemu niliouchagua.
14 Ndipo BWANA akamwondokeshea Sulemani adui, Hadadi Mwedomi; yeye alikuwa wa wazao wake mfalme wa Edomu.
15 Kwa maana ikawa, Daudi alipokuwako Edomu, naye Yoabu, mkuu wa jeshi, amepanda awazike waliouawa, akiisha kumpiga kila mwanamume wa Edomu,
16 (kwa kuwa Yoabu alikaa huko miezi sita pamoja na Israeli wote, hata alipompoteza kila mwanamume wa Edomu);
17 yule Hadadi alikimbia, yeye na Waedomi wengine, watumishi wa baba yake, pamoja naye, waende Misri; yule Hadadi akali ni mtoto mdogo.
18 Wakaondoka katika Midiani, wakafika Parani; wakachukua pamoja nao watu toka Parani, wakafika Misri, kwa Farao mfalme wa Misri; aliyempa nyumba, akamwamria vyakula, akampa mashamba.