5 Madhabahu ikapasuka, majivu ya madhabahuni yakamwagika, sawasawa na ishara aliyoitoa mtu wa Mungu kwa neno la BWANA.
6 Mfalme akajibu, akamwambia yule mtu wa Mungu, Umsihi sasa BWANA, Mungu wako, ukaniombee, ili nirudishiwe mkono wangu tena. Yule mtu wa Mungu akamwomba BWANA mkono wa mfalme ukarudishwa tena, ukawa kama ulivyokuwa kwanza.
7 Mfalme akamwambia mtu wa Mungu, Karibu nyumbani kwangu ujiburudishe, nami nitakupa thawabu.
8 Mtu wa Mungu akamwambia mfalme, Ujaponipa nusu ya nyumba yako, sitaingia pamoja nawe, wala sitakula chakula, wala sitakunywa maji mahali hapa;
9 maana ndivyo nilivyoagizwa kwa neno la BWANA, kusema, Usile chakula cho chote wala usinywe maji, wala usirudi kwa njia ile uliyoijia.
10 Basi akaenda zake kwa njia nyingine, wala hakurudi kwa njia ile aliyoijia Betheli.
11 Basi nabii mmoja mzee alikuwa akikaa katika Betheli; na wanawe wakamwendea wakamwambia kila neno alilolitenda yule mtu wa Mungu siku ile katika Betheli; na maneno aliyomwambia mfalme, hayo nayo walimwambia baba yao.