2 Yeroboamu akamwambia mkewe, Ondoka, tafadhali, ujibadilishe, wasikujue kuwa mkewe Yeroboamu; ukaende Shilo; tazama, yuko huko Ahiya nabii, aliyeninena mimi ya kwamba nitakuwa mfalme juu ya watu hawa.
3 Twaa mkononi mikate kumi, na kaki, na mtungi wa asali, ukamwendee; naye atakuambia kijana atakuwaje.
4 Akafanya hivi mkewe Yeroboamu, akaondoka, akaenda Shilo, akaja nyumbani kwa Ahiya. Basi Ahiya hakuweza kuona; kwa kuwa macho yake yamepofuka kwa sababu ya uzee wake.
5 BWANA akamwambia Ahiya, Angalia, mkewe Yeroboamu anakuja akuulize mambo ya mwanawe; kwa maana hawezi; hivi na hivi umwambie; kwani itakuwa akiingia atajifanya kuwa mwanamke mwingine.
6 Ikawa, Ahiya alipoisikia sauti ya miguu yake, akiingia mlangoni, alisema, Karibu, mkewe Yeroboamu; mbona wajifanya kuwa mwingine maana nimetumwa kwako wewe, mwenye maneno mazito.
7 Nenda, umwambie Yeroboamu, BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kwa kuwa nilikutukuza miongoni mwa watu, nikakufanya uwe mkuu juu ya watu wangu Israeli,
8 nikaurarulia mbali ufalme utoke nyumba yake Daudi, na kukupa wewe; walakini wewe hukuwa kama mtumishi wangu Daudi, aliyezishika amri zangu, na kunifuata kwa moyo wake wote, asifanye lo lote ila yaliyo mema machoni pangu;