23 Na mambo yote ya Asa yaliyosalia, na nguvu zake zote, na yote aliyoyafanya, na miji aliyoijenga, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda? Lakini alipokuwa mzee alikuwa na ugonjwa wa miguu.
24 Asa akalala na babaze, akazikwa pamoja na babaze mjini mwa Daudi baba yake. Na Yehoshafati mwanawe akatawala mahali pake.
25 Nadabu mwana wa Yeroboamu alianza kutawala juu ya Israeli, mwaka wa pili wa Asa mfalme wa Yuda, akatawala juu ya Israeli miaka miwili.
26 Akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, akaiendea njia ya baba yake, na kosa lake alilowakosesha Israeli.
27 Basi Baasha wa Ahiya, wa mbari ya Isakari, akamfanyia fitina; Baasha akampiga huko Gibethoni ulio wa Wafilisti; kwani Nadabu na Israeli wote walikuwa wakiuhusuru Gibethoni.
28 Mwaka wa tatu wa Asa mfalme wa Yuda Baasha akamwua, akatawala mahali pake.
29 Ikawa mara alipotawala, akawapiga nyumba yote ya Yeroboamu. Hakumwachia Yeroboamu mwenye pumzi ye yote, hata alipomharibu sawasawa na neno la BWANA alilolinena kwa mtumishi wake Ahiya, Mshiloni;