24 Kisha akanunua kilima cha Samaria kwa Shemeri kwa talanta mbili za fedha; akajenga juu ya kilima kile, akauita mji alioujenga Samaria, kwa kuliandama jina lake Shemeri, aliyekuwa mwenye kilima.
25 Omri akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA, akatenda maovu kuliko wote waliomtangulia;
26 kwa kuwa aliiendea njia yote ya Yeroboamu mwana wa Nebati, na makosa yake, aliyowakosesha Israeli, ili kumghadhibisha BWANA, Mungu wa Israeli, kwa matendo yao ya ubatili.
27 Nayo mambo yote ya Omri yaliyosalia aliyoyatenda, na uthabiti alioufanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli?
28 Omri akalala na babaze, akazikwa huko Samaria; na Ahabu mwanawe akatawala mahali pake.
29 Ahabu mwana wa Omri alianza kutawala juu ya Israeli katika mwaka wa thelathini na nane wa Asa mfalme wa Yuda; akatawala Ahabu mwana wa Omri juu ya Israeli katika Samaria miaka ishirini na miwili.
30 Ahabu mwana wa Omri akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA kuliko wote waliomtangulia.