2 Basi Eliya akaenda ili ajionyeshe kwa Ahabu. Na njaa ilikuwa nzito katika Samaria.
3 Ahabu akamwita Obadia, aliyekuwa juu ya nyumba yake; (na huyu Obadia alikuwa mwenye kumcha BWANA sana;
4 kwa kuwa ikawa, Yezebeli alipowaua manabii wa BWANA, Obadia akatwaa manabii mia, akawaficha hamsini hamsini katika pango, akawalisha chakula na kuwapa maji).
5 Ahabu akamwambia Obadia, Pita katika nchi, kwenye chemchemi zote za maji, na vijito vyote; labda tutapata majani, tuwahifadhi hai farasi na nyumbu, tusipate hasara ya hao wanyama wote.
6 Basi wakaigawanya nchi, ili wapite katika nchi yote; Ahabu akaenda zake njia moja peke yake, na Obadia akaenda zake njia nyingine peke yake.
7 Na Obadia alipokuwa njiani, kumbe! Eliya akakutana naye. Akamtambua, akaanguka kifudifudi, akanena, Je! Ni wewe, bwana wangu Eliya?
8 Akamjibu, Ni mimi. Enenda, umwambie bwana wako, Tazama, Eliya yupo.