28 Wakapiga kelele, wakajikata-kata kwa visu na vyembe kama ilivyo desturi yao, hata damu ikawachuruzika.
29 Ikawa, wakati wa adhuhuri ulipopita, walitabiri hata wakati wa kutoa dhabihu ya jioni; lakini hapakuwa na sauti, wala aliyejibu, wala aliyeangalia.
30 Kisha Eliya akawaambia watu wote, Nikaribieni mimi. Watu wote wakamkaribia. Akaitengeneza madhabahu ya BWANA iliyovunjika.
31 Eliya akatwaa mawe kumi na mawili, kwa hesabu ya kabila za wana wa Yakobo, aliyejiliwa na neno la BWANA na kuambiwa, Jina lako litakuwa Israeli.
32 Naye akaijenga madhabahu kwa mawe hayo katika jina la BWANA; akafanya mfereji, kama wa vipimo viwili vya mbegu, ukiizunguka madhabahu.
33 Kisha akazipanga zile kuni, akamkata yule ng’ombe vipande vipande, akaviweka juu ya kuni. Akasema, Jazeni mapipa manne maji, mkayamwage juu ya sadaka ya kuteketezwa, na juu ya kuni.
34 Akasema, Fanyeni mara ya pili. Wakafanya mara ya pili. Akasema, Fanyeni mara ya tatu. Wakafanya mara ya tatu.