1 Basi, Ben-hadadi mfalme wa Shamu akakusanya jeshi lake lote; nao walikuwapo wafalme thelathini na wawili pamoja naye, na farasi, na magari: akakwea akauhusuru Samaria, akaupiga vita.
2 Akatuma wajumbe kwa Ahabu mfalme wa Israeli, mjini, akamwambia, Ndivyo asemavyo Ben-hadadi.
3 Fedha yako na dhahabu yako ni zangu mimi; na wakezo na wanao, walio wema, ni wangu.
4 Mfalme wa Israeli akajibu, akasema, Ni kama ulivyosema, bwana wangu, mfalme; mimi ni wako, na vyote nilivyo navyo.
5 Wajumbe wakarudi tena, wakasema, Ndivyo asemavyo Ben-hadadi, Hakika nimetuma kwako kusema, Fedha yako, na dhahabu yako, na wake zako, na wanao, utanitolea mimi;
6 lakini kesho kama wakati huu nitatuma kwako watumwa wangu, ili watazame-tazame nyumba yako na nyumba za watumwa wako; na itakuwa kila kipendezacho machoni pako watakitia mikononi mwao, na kukichukua.