37 Ndipo akaona mtu mwingine, akasema, Nipige, nakusihi. Yule mtu akampiga, hata kumpiga na kumtia jeraha.
38 Basi yule nabii akaenda akamngoja mfalme njiani, amejibadilisha kwa kilemba juu ya macho yake.
39 Ikawa mfalme alipopita, alimwita mfalme; akasema, Mtumwa wako aliingia katikati ya pigano; na tazama, mtu mmoja akanigeukia akaniletea mtu, akaniambia, Umlinde mtu huyu; akipotea kwa njia yo yote, roho yako itakuwa mahali pa roho yake, au utatoa talanta ya fedha.
40 Ikawa mtumishi wako alipokuwa akitenda haya na haya, yule akaenda zake. Mfalme wa Israeli akamwambia, Ndivyo itakavyokuwa hukumu yako; umejihukumu mwenyewe.
41 Akafanya haraka akakiondoa kilemba machoni mwake, mfalme wa Israeli akamtambua kuwa ni mmoja wao manabii.
42 Akamwambia, BWANA asema hivi, Kwa sababu umemwachilia atoke mkononi mwako mtu niliyemweka ili aangamizwe kabisa, roho yako itakuwa mahali pa roho yake, na watu wako mahali pa watu wake.
43 Mfalme wa Israeli akaenda nyumbani kwake na moyo mzito, mwenye hasira, akaja Samaria.