5 Wajumbe wakarudi tena, wakasema, Ndivyo asemavyo Ben-hadadi, Hakika nimetuma kwako kusema, Fedha yako, na dhahabu yako, na wake zako, na wanao, utanitolea mimi;
6 lakini kesho kama wakati huu nitatuma kwako watumwa wangu, ili watazame-tazame nyumba yako na nyumba za watumwa wako; na itakuwa kila kipendezacho machoni pako watakitia mikononi mwao, na kukichukua.
7 Ndipo mfalme wa Israeli, akawaita wazee wote wa nchi, akasema, Angalieni, nawaomba, mwone, kwamba huyu ataka madhara; maana ametuma kwangu kutaka wake zangu na watoto wangu; na fedha yangu na dhahabu yangu, sikumkatalia.
8 Wakamwambia wazee wote na watu wote, Usisikie, wala usikubali.
9 Kwa hiyo akawaambia wale wajumbe wa Ben-hadadi, Mwambieni bwana wangu mfalme, Kila uliyotuma kumtakia mtumwa wako kwanza, nitafanya, ila neno hili siwezi kulifanya. Basi wajumbe wakaenda zao, wakamrudishia maneno hayo.
10 Ndipo Ben-hadadi akatuma kwake, akasema, Miungu wanifanyie hivi na kuzidi, yakiwa mavumbi ya Samaria yatatosha makonzi ya watu wote walio miguuni pangu.
11 Mfalme wa Israeli akajibu, akasema, Mwambieni, Avaaye asijisifu kama avuaye.