4 Ila leo BWANA, Mungu wangu, amenipa amani kila upande; hakuna adui, wala tukio baya.
5 Nami, tazama, nakusudia kujenga nyumba kwa jina la BWANA, Mungu wangu, kama BWANA alivyomwambia Daudi baba yangu, akisema, Mwana wako, nitakayemweka katika kiti chake cha enzi mahali pako, ndiye atakayeijenga nyumba kwa jina langu.
6 Basi uamuru wanikatie mierezi ya Lebanoni; na watumishi wangu watafuatana na watumishi wako; na ujira wa watumishi wako nitakupa kama utakavyosema; kwa kuwa wajua ya kwamba hakuna kwetu mtu ajuaye kukata miti kama Wasidoni.
7 Ikawa, Hiramu aliposikia maneno yake Sulemani, alifurahi sana, akasema, Na ahimidiwe BWANA leo, aliyempa Daudi mwana mwenye akili juu ya watu hawa walio wengi.
8 Hiramu akatuma watu kwa Sulemani, akasema, Nimeyasikia yale uliyoniletea; nami nitafanya kila ulitakalo katika habari ya miti ya mierezi, na miti ya miberoshi.
9 Watumishi wangu wataishusha toka Lebanoni mpaka baharini; nami nitaiendesha baharini, ikifungwa pamoja, mpaka mahali utakaponiagiza, huko nitaifungua ili wewe uichukue; ndivyo utakavyoitimiza haja yangu, ukiwapa chakula watu wa nyumbani mwangu.
10 Basi Hiramu akampa Sulemani miti ya mierezi na miti ya miberoshi kadiri alivyotaka.