21 Akazisimamisha nguzo ukumbini pa hekalu; akaisimamisha nguzo ya kuume, akaiita jina lake Yakini; akaisimamisha nguzo ya kushoto, akaiita jina lake Boazi.
22 Na juu ya nguzo kulikuwa na kazi ya mayungi; hivyo mambo ya nguzo yakatimia.
23 Tena akaifanya bahari ya kusubu, mikono kumi toka ukingo hata ukingo, ikaviringana, na mikono mitano ilikuwa kwenda juu kwake; na uzi wa mikono thelathini kuizunguka kabisa.
24 Na chini ya ukingo wake kulikuwa na maboga yaliyoizunguka, kwa mikono kumi, yakiizunguka bahari; kulikuwa na safu mbili za hayo maboga, yakafanywa kalibuni hapo bahari ilipofanywa.
25 Ikakaa juu ya ng’ombe kumi na wawili, watatu wakitazama kaskazini, na watatu wakitazama magharibi, na watatu wakitazama kusini, na watatu wakitazama mashariki; na bahari iliwekwa juu yao, na pande zao za nyuma zote zilikuwa ndani.
26 Na unene wake ulikuwa nyanda nne; na ukingo wake ukafanywa kama ukingo wa kikombe, kama ua la yungi; huingia bathi elfu mbili.
27 Akayafanya yale matako kumi ya shaba; mikono minne urefu wa tako moja, na mikono minne upana wake, na mikono mitatu kwenda juu kwake.