8 Nayo nyumba yake atakayokalia, katika behewa nyingine iliyokuwa ndani kupita baraza, ilikuwa ya kazi kama hiyo. Tena akamjengea nyumba binti Farao, (ambaye Sulemani alikuwa amemwoa), mfano wa ile baraza.
9 Hizi zote zilikuwa za mawe ya thamani, mawe ya kuchongwa, sawasawa na cheo, yaliyokatwa kwa misumeno, ndani na nje, tangu msingi hata mawe ya juu, na nje vile vile hata behewa kuu.
10 Nao msingi ulikuwa wa mawe ya thamani, mawe makubwa, mawe mikono kumi, na mawe ya mikono minane.
11 Na juu kulikuwa na mawe ya thamani, mawe ya kuchongwa, sawasawa na cheo, na mierezi.
12 Na behewa kubwa pande zote ilikuwa na safu tatu za mawe ya kuchongwa, na safu moja ya mihimili ya mierezi; mfano wa behewa ya ndani ya nyumba ya BWANA, na ukumbi wa nyumba.
13 Mfalme Sulemani akatuma watu kumleta Huramu kutoka Tiro.
14 Naye alikuwa mwana wa mwanamke mjane wa kabila ya Naftali, na babaye alikuwa mtu wa Tiro, mfua shaba; naye alikuwa mwingi wa hekima na akili, mstadi wa kufanya kazi zote za shaba. Akamfikilia mfalme Sulemani, akamfanyia kazi yake yote.