5 Daudi akasema, Sulemani mwanangu akali ni mchanga bado, na mwororo, nayo nyumba atakayojengewa BWANA haina budi kuwa nzuri mno, yenye sifa na yenye fahari katika nchi zote; kwa hiyo mimi nitaiwekea akiba. Basi Daudi akaweka akiba tele kabla hajafa.
6 Ndipo akamwita Sulemani mwanawe, akamwagiza amjengee BWANA, Mungu wa Israeli, nyumba.
7 Daudi akamwambia Sulemani mwanawe, Kwangu mimi nia yangu ilikuwa kujenga nyumba kwa ajili ya jina la BWANA, Mungu wangu.
8 Lakini neno la BWANA likanijia, kusema, Wewe umemwaga damu nyingi, na vita vikubwa umevifanya; wewe hutajenga nyumba kwa ajili ya jina langu, kwa sababu umemwaga damu nyingi juu ya nchi machoni pangu;
9 tazama, utazaliwa mwana, atakayekuwa mtu wa kustarehe; nami nitamstarehesha mbele ya adui zake pande zote; kwani jina lake litakuwa Sulemani, nami nitawapa Israeli amani na utulivu siku zake;
10 huyo ndiye atakayejenga nyumba kwa ajili ya jina langu; naye atakuwa mwanangu, nami nitakuwa babaye; nami nitakifanya imara milele kiti cha ufalme wake juu ya Israeli.
11 Sasa mwanangu, BWANA na awe pamoja nawe; ukafanikiwe, na kuijenga nyumba ya BWANA, Mungu wako, kama alivyonena kwa habari zako.