35 Naye Sauli akamjengea BWANA madhabahu; hiyo ndiyo madhabahu ya kwanza aliyomjengea BWANA.
36 Kisha Sauli akasema, Haya! Na tushuke kuwafuata Wafilisti wakati wa usiku, na kuwateka nyara hata mapambazuko, wala tusiwaache hata mmoja wao. Nao wakamjibu, Fanya yo yote uyaonayo kuwa ni mema. Ndipo yule kuhani akasema, Na tumkaribie Mungu hapa.
37 Basi Sauli akataka shauri kwa Mungu, Je! Nishuke ili kuwafuatia Wafilisti? Je! Utawatia mikononi mwa Israeli? Lakini hakumjibu neno lo lote siku ile.
38 Ndipo Sauli akasema, Karibieni hapa, enyi wakuu wote wa watu; mjue na kuona dhambi hii ya leo imekuwa katika kosa gani.
39 Kwa maana, aishivyo BWANA, awaokoaye Israeli, ijapokuwa i katika Yonathani, mwanangu, kufa atakufa. Lakini miongoni mwa watu wote hakuna mtu ye yote aliyemjibu.
40 Ndipo akawaambia Israeli wote, Ninyi mtakuwa upande mmoja, na mimi na mwanangu Yonathani tutakuwa upande wa pili. Basi wakamwambia Sauli, Fanya uonayo kuwa ni mema.
41 Kwa hiyo Sauli akamwambia BWANA, Mungu wa Israeli, [Kwani usimjibu mtumishi wako leo? Ikiwa dhambi i ndani yangu, au ndani yake Yonathani mwanangu, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, utoe Urimu; bali ukisema hivi, Dhambi i katika watu wako Israeli,] utoe Thumimu. Basi Yonathani na Sauli wakatwaliwa, lakini watu wakapona.