40 Ndipo akawaambia Israeli wote, Ninyi mtakuwa upande mmoja, na mimi na mwanangu Yonathani tutakuwa upande wa pili. Basi wakamwambia Sauli, Fanya uonayo kuwa ni mema.
41 Kwa hiyo Sauli akamwambia BWANA, Mungu wa Israeli, [Kwani usimjibu mtumishi wako leo? Ikiwa dhambi i ndani yangu, au ndani yake Yonathani mwanangu, Ee BWANA, Mungu wa Israeli, utoe Urimu; bali ukisema hivi, Dhambi i katika watu wako Israeli,] utoe Thumimu. Basi Yonathani na Sauli wakatwaliwa, lakini watu wakapona.
42 Basi Sauli akasema, Sasa piga kati ya mimi na mwanangu Yonathani, [naye awaye yote ambaye BWANA atamtwaa, atakufa. Nao watu wakamwambia Sauli, La! Sivyo hivyo; lakini Sauli akawaweza watu. Nao wakapiga kati ya yeye na mwanawe Yonathani,] naye Yonathani akatwaliwa.
43 Ndipo Sauli akamwambia Yonathani, Niambie ulilolifanya. Basi Yonathani akamwambia, akasema, Ni kweli, mimi nalionja asali kidogo kwa ncha ya fimbo ile iliyokuwa mkononi mwangu; na tazama, imenipasa kufa.
44 Naye Sauli akasema, Mungu anifanyie hivi, na kuzidi; kwa kuwa hakika utakufa, Yonathani.
45 Walakini watu wakamwambia Sauli, Je! Atakufa Yonathani, ambaye ndiye aliyeufanya huo wokovu mkuu katika Israeli? Hasha! Aishivyo BWANA, hautaanguka chini hata unywele mmoja wa kichwa chake; kwa maana ametenda kazi pamoja na Mungu leo. Hivyo hao watu wakamponya Yonathani, asife.
46 Ndipo Sauli akakwea kuacha kuwafuata Wafilisti; nao Wafilisti wakaenda zao kwao.