2 BWANA wa majeshi asema hivi, Nimeyatia moyoni mwangu mambo hayo Amaleki waliyowatenda Israeli, jinsi walivyowapinga njiani, hapo walipopanda kutoka Misri.
3 Basi sasa enda ukawapige Amaleki, na kuviharibu kabisa vitu vyote walivyo navyo, wala msiwaachilie; bali waueni, mwanamume na mwanamke, mtoto naye anyonyaye, ng’ombe na kondoo, ngamia na punda.
4 Ndipo Sauli akawaita watu, akawahesabu huko Telemu, askari waliopanda farasi mia mbili elfu, na watu wa Yuda kumi elfu.
5 Sauli akaufikilia mji wa Amaleki, akauvizia bondeni.
6 Sauli akawaambia Wakeni, Haya! Enendeni zenu, mkashuke ili kujitenga na Waamaleki, nisije nikawaangamiza ninyi pamoja nao; maana mliwatendea wana wa Israeli mema, walipopanda kutoka Misri. Basi hao Wakeni wakaondoka, wakajitenga na Waamaleki.
7 Sauli akawapiga Waamaleki, toka Havila uendapo Shuri, unaokabili Misri.
8 Akamkamata Agagi, mfalme wa Waamaleki, yu hai, akawaangamiza hao watu wote kwa upanga.