20 Daudi akaondoka asubuhi na mapema, akawaacha kondoo pamoja na mchungaji, akavitwaa vitu vile, akaenda, kama Yese alivyomwamuru; akafika penye magari, wakati lile jeshi walipokuwa wakitoka kwenda kupigana, wakipiga kelele za vita.
21 Nao Waisraeli na Wafilisti wakajipanga, jeshi hili likikabili jeshi hili.
22 Basi Daudi akaviacha vile vyombo vyake katika mkono wa mlinda vyombo, akalikimbilia jeshi, akafika, akawasalimu ndugu zake.
23 Hata alipokuwa akisema nao, kumbe! Yule shujaa alitokea, yule Mfilisti wa Gathi, jina lake Goliathi, akitoka katika jeshi la Wafilisti, akasema maneno yale yale; naye Daudi akayasikia.
24 Na watu wote wa Israeli walipomwona yule mtu wakakimbia, wakaogopa sana.
25 Watu wa Israeli wakasema, Je! Mmemwona mtu huyu aliyepanda huko? Hakika ametokea ili awatukane Israeli; basi, itakuwa, mtu yule atakayemwua, mfalme atamtajirisha kwa utajiri mwingi, naye atamwoza binti yake, na kuifanya mbari ya baba yake kuwa huru katika Israeli.
26 Daudi akaongea na watu waliosimama karibu, akisema, Je! Atafanyiwaje yeye atakayemwua Mfilisti huyo, na kuwaondolea Israeli aibu hii? Maana Mfilisti huyu asiyetahiriwa ni nani hata awatukane majeshi ya Mungu aliye hai?