39 Naye Daudi akajifunga upanga juu ya mavazi yake, akajaribu kwenda; maana alikuwa hajavijaribu. Daudi akamwambia Sauli, Siwezi kwenda na vitu hivi, maana sikuvijaribu. Basi Daudi akavivua.
40 Akaichukua fimbo yake mkononi, akajichagulia mawe laini matano katika kijito cha maji, akayatia katika mfuko wa kichungaji aliokuwa nao, maana ni mkoba wake, na kombeo lake alikuwa nalo mkononi mwake, akamkaribia yule Mfilisti.
41 Huyo Mfilisti naye akamsogelea Daudi na kumkaribia; na mtu yule aliyemchukulia ngao yake akamtangulia.
42 Hata Mfilisti alipotazama huku na huku, akamwona Daudi akamdharau; kwa kuwa ni kijana tu mwekundu, tena ana sura nzuri.
43 Mfilisti akamwambia Daudi, Je! Mimi ni mbwa hata umenijia kwa fimbo? Mfilisti akamlaani Daudi kwa miungu yake.
44 Mfilisti akamwambia Daudi, Njoo huku kwangu; nyama yako nitawapa ndege wa angani na wanyama wa mwituni.
45 Ndipo Daudi akamwambia yule Mfilisti, Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la BWANA wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli uliowatukana.