11 kisha wakaliweka sanduku la BWANA juu ya gari, pamoja na kasha lenye panya wa dhahabu na sanamu za majipu yao.
12 Na hao ng’ombe wakashika njia moja kwa moja kwenda Beth-shemeshi; wakaiandama njia ya barabara, wakaenda wakilia, lakini hawakugeukia upande wa kuume wala wa kushoto; na mashehe wa Wafilisti wakawafuata hata kuufikia mpaka wa Beth-shemeshi.
13 Nao watu wa Beth-shemeshi walikuwa wakivuna ngano yao bondeni; wakainua macho yao, wakaliona sanduku, wakafurahi sana kuliona.
14 Na lile gari likaingia katika konde la Yoshua wa Beth-shemeshi, na kusimama pale pale, palipokuwapo jiwe kubwa; basi wakaipasua miti ya lile gari, wakawatoa wale ng’ombe kuwa ni sadaka ya kuteketezwa kwa BWANA.
15 Nao Walawi walilishusha sanduku la BWANA, na lile kasha lililokuwa pamoja nalo, lenye vile vitu vya dhahabu; wakaviweka juu ya lile jiwe kubwa; nao watu wa Beth-shemeshi wakatoa sadaka za kuteketezwa, na kuchinja dhabihu siku iyo hiyo kwa BWANA.
16 Na hao mashehe watano wa Wafilisti, hapo walipokwisha kuyaona hayo, walirejea Ekroni siku iyo hiyo.
17 Hii ndiyo hesabu ya yale majipu waliyoyapeleka wale Wafilisti, yawe matoleo ya kosa kwa BWANA; kwa Ashdodi moja, kwa Gaza moja, kwa Ashkeloni moja, kwa Gathi moja, na kwa Ekroni moja;