1 Rehoboamu akaenda Shekemu; maana Israeli wote walikuwa wamekuja Shekemu, ili wamfanye mfalme.
2 Ikawa Yeroboamu mwana wa Nebati aliposikia, (maana alikuwako Misri, ambako amekimbilia mbele ya mfalme Sulemani), Yeroboamu akarudi kutoka Misri.
3 Wakapeleka ujumbe, wakamwita, Yeroboamu akaja na Israeli wote, wakamwambia Rehoboamu, wakasema,
4 Baba yako alilifanya zito kongwa letu; basi sasa upunguze utumwa mgumu wa baba yako, na kongwa lake zito alilotutwika, nasi tutakutumikia.
5 Akawaambia, Mnirudie baada ya siku tatu. Watu wakaenda zao.
6 Mfalme Rehoboamu akataka shauri kwa wazee, waliosimama mbele ya Sulemani baba yake, alipokuwa hai bado, akasema, Mwanipa shauri gani la kuwajibu watu hawa?
7 Wakamwambia, wakasema, Ukiwa mwema kwao watu hawa, na kuwapendeza, na kuwaambia maneno mazuri, ndipo watakapokuwa watumishi wako siku zote.