1 Hivyo ikaisha kazi yote Sulemani aliyoifanyia nyumba ya BWANA. Sulemani akaviingiza vitu alivyovitakasa baba yake Daudi; fedha, na dhahabu, na vyombo vyote, akavitia ndani ya hazina za nyumba ya Mungu.
2 Ndipo Sulemani alipowakusanya wazee wa Israeli, na wakuu wote wa kabila, wakuu wa mbari za mababa wa wana wa Israeli, huko Yerusalemu, ili walipandishe sanduku la agano la BWANA kutoka mji wa Daudi, yaani, Sayuni.
3 Wakakutana watu wote wa Israeli mbele ya mfalme wakati wa sikukuu, katika mwezi wa saba.
4 Wakaja wazee wote wa Israeli, nao Walawi wakajitwika sanduku.
5 Wakalipandisha sanduku, na ile hema ya kukutania, na vyombo vitakatifu vyote vilivyokuwamo Hemani, vitu hivyo makuhani Walawi wakavipandisha.
6 Mfalme Sulemani, na mkutano wote wa Israeli, waliokutanika kwake, walikuwako mbele ya sanduku, wakichinja dhabihu za kondoo na ng’ombe, wasiohesabika wala kujumlishwa kwa kuwa wengi.
7 Makuhani wakaliingiza sanduku la agano la BWANA mahali pake katika chumba cha ndani cha nyumba, patakatifu pa patakatifu, yaani, chini ya mabawa ya makerubi.
8 Kwa maana makerubi yalinyosha mabawa yao juu ya mahali pa sanduku, makerubi yakalifunika lile sanduku na miti yake kwa juu.
9 Na ile miti ilikuwa mirefu, hata ncha za miti zilionekana sandukuni mbele ya chumba cha ndani, lakini hazikuonekana nje; nayo iko kuko huko hata leo.
10 Hamkuwa na kitu ndani ya sanduku, ila zile mbao mbili alizozitia Musa huko Horebu, BWANA alipofanya agano na wana wa Israeli, hapo walipotoka Misri.
11 Ikawa makuhani walipokwisha kutoka katika patakatifu; (kwani makuhani wote waliokuwapo, walikuwa wamejitakasa, wala hawakuzishika zamu zao;
12 tena Walawi waimbaji, wote pia, yaani Asafu, na Hemani, na Yeduthuni, na wana wao, na ndugu zao, hali wamevaa kitani safi, wenye matoazi na vinanda na vinubi, wamesimama upande wa mashariki wa madhabahu, na pamoja nao makuhani mia na ishirini wakipiga panda;)
13 hata ikawa, wenye panda na waimbaji walipokuwa kama mmoja, wakisikizisha sauti moja ya kumsifu na kumshukuru BWANA nao wakipaza sauti pamoja na panda na matoazi na vinanda, wakimsifu BWANA, wakisema, Kwa kuwa ni mwema; kwa maana fadhili zake ni za milele; ndipo nyumba ikajawa na wingu, naam, nyumba ya BWANA,
14 hata makuhani hawakuweza kusimama ili kufanya huduma yao, kwa sababu ya lile wingu; kwa kuwa nyumba ya Mungu imejaa utukufu wa BWANA.