1 Basi Sulemani alikusudia kujenga nyumba kwa jina la BWANA, na kuujengea ufalme wake nyumba.
2 Sulemani akahesabu watu sabini elfu wawe wachukuzi wa mizigo, na watu themanini elfu wawe wachongaji milimani, na elfu tatu na mia sita wawe wasimamizi wao.
3 Sulemani akatuma watu kwa Hiramu mfalme wa Tiro, akisema, Kama ulivyomtendea baba yangu Daudi, na kumletea mierezi, ajijengee nyumba ya kukaa, unitendee na mimi.
4 Angalia, najenga nyumba kwa jina la BWANA, Mungu wangu, ili kumfanyia wakfu, ya kufukizia mbele zake fukizo la manukato, na ya mkate wa wonyesho wa daima, na ya sadaka za kuteketezwa za asubuhi na jioni, na za siku za sabato, na za mwezi mpya, na za sikukuu zilizoagizwa za BWANA, Mungu wetu. Hili ni agizo la milele kwa Israeli.
5 Nayo nyumba nitakayoijenga ni kubwa; kwa sababu Mungu wetu ndiye mkuu juu ya miungu yote.
6 Lakini ni nani awezaye kumjengea nyumba, ikiwa mbingu hazimtoshi, wala mbingu za mbingu? Nami ni nani basi, hata nimjengee nyumba, isipokuwa kwa ajili ya kufukizia fukizo mbele zake?
7 Unipelekee basi mtu mstadi wa kazi ya dhahabu, na ya fedha, na ya shaba, na ya chuma, na ya urujuani, na nyekundu, na samawi, mwenye kujua kuchora machoro, pamoja na wastadi walioko Yuda na Yerusalemu pamoja nami, aliowaweka baba yangu Daudi.
8 Niletee tena mierezi, na miberoshi, na miti ya msandali kutoka Lebanoni; maana najua ya kwamba watumishi wako hujua sana kuchonga miti Lebanoni; na tazama, watumishi wangu watakuwa pamoja na watumishi wako,
9 ili wanitengenezee miti kwa wingi; kwani nyumba nitakayoijenga itakuwa kubwa ajabu.
10 Na tazama, nitawapa watumishi wako, wachongaji wakatao miti, kori ishirini elfu za ngano iliyopondwa, na kori ishirini elfu za shayiri, na bathi ishirini elfu za mvinyo na bathi ishirini elfu za mafuta.
11 Ndipo Hiramu mfalme wa Tiro akajibu kwa waraka, aliompelekea Sulemani, Ni kwa sababu BWANA awapenda watu wake, amekufanya uwe mfalme juu yao.
12 Hiramu akasema tena, Na ahimidiwe BWANA, Mungu wa Israeli, aliyezifanya mbingu na nchi, ambaye amempa mfalme Daudi mwana wa hekima, mwenye busara na akili, ili amjengee BWANA nyumba, na nyumba kwa ufalme wake.
13 Na sasa nimemtuma mtu mstadi, mwenye akili, yaani, Hiramu baba yangu,
14 mwana wa mwanamke wa binti za Dani, na babaye alikuwa mtu wa Tiro, ajuaye sana kazi ya dhahabu, na ya fedha, ya shaba, ya chuma, ya mawe, na ya mti, ya urujuani, ya samawi, na ya kitani safi, na ya nyekundu; tena mstadi wa kuchora machoro yo yote, na wa kufikiri fikira yo yote; apate kuagiziwa kazi pamoja na watu wako wastadi, tena na wastadi wa bwana wangu Daudi baba yako.
15 Basi sasa hiyo ngano na shayiri, mafuta na mvinyo, aliyonena bwana wangu, na wapelekewe watumishi wake;
16 nasi tutakata miti katika Lebanoni, kadiri utakavyohitaji; na kukuletea tukiieleza baharini mpaka Yafa; nawe utaichukua Yerusalemu.
17 Ndipo Sulemani akawahesabu wageni wote waliokuwamo katika nchi ya Israeli, sawasawa na hesabu aliyowahesabu Daudi baba yake; wakatokea mia hamsini na tatu elfu, na mia sita.
18 Akaweka katika hao sabini elfu wawe wachukuzi wa mizigo, na themanini elfu wawe wachongaji milimani, na wasimamizi elfu tatu na mia sita, ili wawatie watu kazini.