2 Naye Sulemani akamfumbulia maswali yake yote; wala halikuwako neno alilofichiwa Sulemani, asimwambie.
3 Naye malkia wa Sheba alipoona hekima ya Sulemani, na nyumba aliyoijenga,
4 na vyakula vya mezani mwake, na kikao cha watumishi wake, na usimamizi wao wangoje wake, na mavazi yao; na wanyweshaji wake, na mavazi yao; na daraja yake ya kupandia mpaka nyumba ya BWANA; roho yake ilizimia.
5 Akamwambia mfalme, Ndizo kweli habari zile nilizozisikia katika nchi yangu za mambo yako na za hekima yako.
6 Lakini mimi sikuyasadiki maneno yao, hata nilipokuja na kuona kwa macho yangu; wala, tazama, ukuu wa hekima yako sikuambiwa nusu; wewe umezidi kuliko habari nilizozisikia.
7 Heri watu wako, na heri hawa watumishi wako, wasimamao mbele yako sikuzote, wakisikia hekima yako.
8 Na ahimidiwe BWANA, Mungu wako, aliyependezwa nawe, ili akuweke juu ya kiti chake cha enzi, kuwa mfalme wake BWANA, Mungu wako; kwa kuwa Mungu wako amewapenda Israeli, kuwathibitisha milele, kwa hiyo amekufanya kuwa mfalme juu yao, ufanye hukumu na haki.