1 Ndipo BWANA akamtuma Nathani aende kwa Daudi. Naye akamwendea, akamwambia, Palikuwa na watu wawili katika mji mmoja; mmoja wao alikuwa tajiri, wa pili maskini.
2 Yule tajiri alikuwa na kondoo na ng’ombe wengi sana;
3 bali yule maskini hakuwa na kitu, ila mwana kondoo mmoja, mdogo, ambaye amemnunua na kumlea; naye akakua pamoja naye, na pamoja na wanawe; hula sehemu ya posho lake, na kukinywea kikombe chake, na kulala kifuani mwake, akawa kwake kama binti.
4 Hata msafiri mmoja akamfikilia yule tajiri, naye akaacha kutwaa mmoja wa kondoo zake mwenyewe au mmoja wa ng’ombe zake mwenyewe, ili kumwandalia yule msafiri aliyemfikilia, bali alimnyang’anya yule maskini mwana-kondoo wake, akamwandalia yule mtu aliyemfikilia.