3 Mfalme akasema, Na mwana wa bwana wako yuko wapi? Siba akamwambia mfalme, Angalia, anakaa Yerusalemu; kwani alisema, Leo nyumba ya Israeli watanirudishia ufalme wa baba yangu.
4 Ndipo mfalme akamwambia Siba, Tazama, yote yaliyokuwa ni mali ya Mefiboshethi ni yako. Siba akasema, Mimi nasujudu; na nione kibali machoni pako, Ee bwana wangu, mfalme.
5 Basi mfalme Daudi alipofika Bahurimu, tazama, kulitoka huko mtu wa jamaa ya nyumba ya Sauli, jina lake akiitwa Shimei, mwana wa Gera; alitoka, akalaani alipokuwa akienda.
6 Tena akamtupia Daudi mawe, na watumishi wote wa mfalme Daudi; na watu wote na mashujaa wote walikuwako mkono wake wa kuume na mkono wake wa kushoto.
7 Na Shimei alipolaani, alisema hivi, Nenda zako! Nenda zako! Ewe mtu wa damu! Ewe mtu usiyefaa!
8 BWANA amerudisha juu yako damu yote ya nyumba ya Sauli ambaye umetawala badala yake; naye BWANA ametia ufalme katika mkono wa Absalomu mwanao; kisha, angalia, wewe umetwaliwa katika uovu wako mwenyewe, kwa sababu umekuwa mtu wa damu.
9 Ndipo Abishai mwana wa Seruya, akamwambia mfalme, Mbona mbwa mfu huyu amlaani mfalme bwana wangu? Na nivuke, nakusihi, nikaondoe kichwa chake.