4 Shauri hili likawa jema machoni pa Absalomu, na machoni pa wazee wote wa Israeli.
5 Ndipo Absalomu akasema, Basi, mwiteni Hushai, Mwarki, naye, tukasikie atakayosema yeye pia.
6 Basi Hushai alipofika kwa Absalomu, Absalomu akamwambia, akasema, Ahithofeli amesema hivi; je! Tufanye kama alivyosema? Kama sivyo, sema maneno yako.
7 Hushai akamwambia Absalomu, Shauri hili alilolitoa Ahithofeli si jema wakati huu.
8 Hushai akafuliza kusema, Wamjua baba yako na watu wake, ya kuwa ni watu mashujaa hawa, nao wana uchungu katika mioyo yao, kama dubu aliyenyang’anywa watoto wake nyikani; tena baba yako ni mtu wa vita, hatalala pamoja na watu wake.
9 Angalia, amefichwa sasa katika shimo, au penginepo; kisha itakuwa, watakapoanguka baadhi yao mwanzo, kila mtu atakayesikia, atasema, Kuna machinjo katika watu wanaofuatana na Absalomu.
10 Basi hata yeye aliye shujaa, mwenye moyo kama moyo wa simba, atayeyuka kabisa; maana Israeli wote wanajua ya kuwa baba yako ni shujaa, na ya kuwa watu wale walio pamoja naye ni mashujaa.